HOTUBA YA
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA
WANANCHI, 28 FEBRUARI, 2013
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na
kutuwezesha kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa
kufanya hivyo kila mwisho wa mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo
matatu; yaani Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha
Nne.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu Wananchi;
Tarehe 8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,
Mhe. Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na
Kusini kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake. Pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola, Zambia na Tanzania ambazo ni jirani
ya Kongo. Nchi za Ethiopia, Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja
wa Mataifa na Umoja wa Afrika zilitia saini kama wadhamini. Ethiopia kwa
nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na Msumbiji kwa kuwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi
wanachama wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo
ni Mwenyekiti wake wa sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa
taifa kubwa na linalotegemewa katika ukanda wetu.
Mpango huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
ipate amani ya kudumu. Kama tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa vita vilivyosababisha
kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo rafiki na jirani
haijapata amani na utulivu wa kudumu. Kumekuwepo jitihada na mipango
kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea
tena na mipango hiyo kuvurugika. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni
5.4 wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi
yao. Pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu Wananchi;
Machafuko yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo
sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa,
Ethiopia tarehe 8 Februari, 2013. Katika Mpango huo Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana
kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi zetu.
Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au kwa kutumia watu
wengine. Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu kutumia
nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine. Kimsingi tumekubaliana
kuwa majirani wema. Katika Mkataba huo, majukumu ya kila nchi
yameainishwa vizuri pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na
Mashirika ya Kikanda hususan SADC na ICGLR.
Ndugu Wananchi;
Niliamua kukubali kushiriki na kutia saini Mpango ule kwa kutambua ukweli
kwamba sisi majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia kwa kile
tunachoweza. Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama
Mpango huu utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga mkono.
Ni kwa misingi hiyo hiyo, tulikubali kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi la
Kimataifa la kulinda amani huko Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa na
Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwezi Julai, 2012. Uamuzi huo umeungwa
mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika. Umoja wa Mataifa umeamua Jeshi hilo liwe sehemu ya Jeshi la
Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani nchini Kongo (MONUSCO) jambo ambalo sote
tumeliafiki. Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa
nini tusipeleke Kingo. Miaka ya nyuma tulishapeleka walinzi wa amani
Liberia, Siera Leon na Eritrea.
Ni matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa
matunda yaliyokusudiwa. Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa kwetu. Ina
maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa
Tanganyika kutokuwepo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa
upande wetu na wao. Ni chachu muhimu ya maendeleo ya Mikoa ya pembeni mwa
Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo
Ndugu wananchi;
Jambo la pili
ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa
nchini. Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana kumekuwepo na matukio
kadhaa yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini
ya Kikristo na Kiislamu. Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini za
wengine, kunajisi vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada
na mzozo kuhusu nani achinje. Kumekuwepo na matumizi mabaya
ya radio na simu za mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano iliyoeneza
maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini zetu hizi
kubwa hapa nchini. Kauli na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo
yamekuwa chanzo cha uhasama na magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha
vifo kama ilivyotokea Buseresere Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu zangu;
Watanzania hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote
Watanzania ni watu tunaotambua na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali
tunazoabudu. Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa
tunavumiliana kwa tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu,
kwa umoja na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati
kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na
taratibu ya dini yake.
Watanzania wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba moja,
wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na
ushirikiano. Kuna koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine
Waislamu na wengine Wakristo. Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa
na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake. Wapo pia
ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto na wanashirikiana kulea watoto wao.
Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu
tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi
na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.
Ndugu Wananchi;
Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa
wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri. Tusiwape nafasi
wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na
nchi yetu. Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote
wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine
na wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye
matukio ya namna hiyo. Wawachukulie hatua stahiki wale wote
wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi
nyumba ya njaa”. Wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini
wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na
hatia. Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi wa amani wa
maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao. Pia nimewataka
Polisi wakamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika
wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ndugu Wananchi;
Naendelea kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu
ya wajibu wao maalum wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya
tatizo na mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini. Hali
kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na wenzao wa
upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano mwema baina
yao.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na
mbomoa nchi ni mwananchi”. Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali
kuwa wabomoa nchi. Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi
wapi? Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.
Kwa mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole
makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri
Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa
wao. Serikali na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika
kipindi hiki kugumu. Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini
wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa
kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe
kwa amani roho za viongozi wetu. Amin.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012. Wanafunzi 397,132
walifanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na
asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903 ambao ni sawa na asilimia 65.5
hawakufaulu mtihani huo. Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni mabaya kuliko
matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2011, jumla ya wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo na waliofaulu
walikuwa asilimia 53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia
46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya wanafunzi hao walifaulu na asilimia 49.6
ya wanafunzi hawakufaulu.
Ndugu Wananchi;
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua
na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki kabisa. Kwanza,
kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6
mwaka 2011 hadi asilimia 34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1
ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana. Pili, kwamba hata shule
zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule
za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo
hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii
hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao. Nazo zimejikuta zikiwa na
idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la pili na la tatu ikipungua
wakati waliopata daraja la nne na waliofeli wakiongezeka.
Isitoshe na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua pia. Mwaka 2010
wanafunzi 10 bora wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama au
pointi 7. Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la
kwanza kwa alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi
10 bora, watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 na
wawili alama 11.
Ndugu Wananchi;
Haya ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa
majawabu ya uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo msingi wa uamuzi wa
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima
la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake. Hali hii haijawahi kutokea
katika miaka ya hivi karibuni. Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi
yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika. Hii itawezesha
Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo mapema
iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni. Tusipofanya
hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa
Serikali.
Ndugu Wananchi;
Hivi sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini
matokeo yamekuwa mabaya. Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika utungaji
wa mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. Wapo
wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo au baadhi yao kutokumudu masomo
wanayofundisha. Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika
kufuatilia masomo na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao
shuleni. Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera, mitaala na
uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu. Wapo
wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia
100 kama walivyotaka imechangia. Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana
mawazo yake. Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa tunadhani kwa sababu
tunayo dhamana maalum. Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana
kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe
kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa
kipaumbele cha juu sana kwa elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa
upande wangu na wenzangu wote Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana na
matokeo haya. Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na
asilimia 24 ya bajeti yote ya Serikali ndiyo kubwa kuliko zote. Kwa ajili
hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi mkubwa
wa elimu ya sekondari na elimu ya juu. Bado hatujazimaliza changamoto
zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu, lakini mafanikio yanaendelea
kupatikana. Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo
itakapofikia mahali kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!